Taharuki, tafakuri, mijadala, utani na sintofahamu ilizuka jana baada ya bundi kuwahi namba ndani ya ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kujitwalia eneo la juu akisoma kila namba ya viti vya waheshimiwa.
Maafisa wa Bunge waliamua kuhangaika na bundi mapema kabla hajatia doa kibarua chao kwani mgeni huyu hata kitabu cha wageni hajasaini!
Baada ya Spika, Job Ndugai kuingia, aliwatuliza wabunge kuwa ndege huyo hana madhara anapoonekana mchana, kwa Dodoma. Wagogo tupo?!
“Waheshimiwa wabunge, asubuhi tumeanza kumuona bundi ndani ya jengo hili. Lakini kwa Dodoma, Bundi wa mchana hana madhara kwa hiyo ni mambo ya kawaida kabisa,” alisema Spika Ndugai.
Kupitia makala hii fupi iliyoandikwa na Ghati na kusimiliwa na Mercy Mbaya, utafahamu mambo mengi ya kustaajabisha kuhusu bundi. Ni ndege ambaye amefanya mengi kwenye hii dunia, ametukuzwa sana hadi picha yake kuwekwa kwenye pesa, ametumika vitani. Amewahi kuaminika kuwa chanzo cha busara na hekima. Pia, amewahi kuwa alama ya bahati na unabii.