Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema amesema kuwa kama Waziri wa Mambo ya Ndani wa sasa Kangi Lugola akijitahidi ataweza kuvaa viatu vya enzi zake mwaka 1990.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, ambapo amesema kuwa Rais Dkt. Magufuli amepata Waziri mzuri ambaye ataweza kusafisha nchi kama ataweza kuendelea na mwendo alio nao sasa.
“Rais Magufuli kampata Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola anayefanya vizuri na ninaweza nikasema akiendelea hivi ataweza kuvivaa viatu vyangu kwasababu Wizara ya Mambo ya Ndani ndio kioo na taa. Uchafu wowote ambao unataka kuondoshwa kwenye nchi lazima Wizara ya Mambo ya Ndani ishughulike nao,”amesema Mrema
Aidha, mwaka 1990, wakati wa serikali ya awamu ya pili, Augustine Mrema aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani hadi mwaka 1994 ambapo alibadilishwa Wizara hiyo na kuhamishiwa katika Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo
Hata hivyo, Mrema amempongeza Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kwa kubaini upotevu wa Mbwa wa Polisi anayejulikana kwa jina la ‘hobby’ wakati alipokuwa kwenye ziara yake katika Kikosi cha Farasi na Mbwa kilichopo eneo la Bandari Jijini Dar es Salaam na kumuagiza IGP Sirro kutoa maelezo ya upotevu wa Mbwa huyo.