Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC kiepongeza hatua zinazochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli za kuzuia mchanga wa dhahabu kusafirishwa kupelekwa nje ya nchi na kuwashughuikia wale wote waliohusika.
Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi wa kituo hicho, Anna Henga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa wao kama kituo cha sheria na watetezi wa haki za binadamu wanaunga mkono hatua hizo kwani taifa lilikuwa linaibiwa rasilimali nyingi.
Aidha, ameitaka Serikali iunde tume ya mamlaka kamili ya madini itakayokuwa inafanya kazi ya uratibu ya shughuli zote za madini Tanzania kama zilivyo mamlaka za hifadhi ya jamii.
“Serikali iwachukulie hatua wale wote waliotajwa katika ripoti za kamati zote mbili na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kujibu tuhuma zao bila kujali vyeo vyao, nafasi zao, kazi zao na nafasi zao katika jamii,”amesema Henga.
Hata hivyo, Henga ameitaka Serikali kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo wadogo wa ndani ili kuanzisha soko rasmi la wachimbaji wadogo wadogo wanazalisha na wachimbaji hao katika maeneo tofauti tofauti hapa nchini.