Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini, Prof. Ibrahim Lipumba amemtuhumu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif kuwa yeye ndiye tatizo na chanzo cha mgogoro.
Amesema kuwa Katibu Mkuu huyo amekuwa anakiendesha chama kisulutani kwa matakwa yake binafsi bila kuangalia katiba inasemaje.
Ameyasema hayo wakati akizungumza katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Cloudstv, Lipumba amesema kuwa ameshamtumia barua Maalim Seif ya kumtaka kuripoti ofisi kuu zilizopo Buguruni lakini amekaidi agizo hilo.
“Chanzo cha mgogoro huu ni Maalim na wala sio Ukawa kama watu wanavyosema, nimefanya kila jitihada za kumaliza mgogoro huu lakini Katibu hataki kunisikiliza,”amesema Lipumba.
Aidha, Lipumba ameyasema hayo mara baada ya Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif kusema kuwa Mwenyekiti huyo alishafukuzwa uanachama ndani ya chama hicho.
Hata hivyo, Lipumba ameongeza kuwa aliamua kuchukua hatua hiyo ya kurudi katika nafasi ya Uenyekiti ndani ya chama hicho ili kuweza kukinusuru chama.