Rais wa wanasheria Tanzania, (TLS) na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amejibu tuhuma zilizotolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya CZI inayomiliki gazeti la Tanzanite, Cyprian Majura Musiba kuwa ni mmoja kati ya watu hatarishi Tanzania
Lissu amejibu tuhuma hizo alipofanya mahojiano maalumu na Dar24 akiwa Ubelgiji anakofanyiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.
Katika mahojiano hayo, Lissu amesema kuwa yeye ni mpinzani wa serikali ambayo imeruhusu upinzani kikatiba na kisheria hivyo anachokifanya yeye ni kuipinga Serikali ya Magufuli (CCM).
Aidha ameongezea kuwa yeye pamoja na wote waliotajwa katika sakata hilo sio maadui wa Taifa, bali ni maadui wa Serikali ya CCM inayoongozwa na Magufuli.
”Sasa kuwa mpinzani wa serikali ya magaufuli kama ilivyokuwa ya kikwete na mkapa hiyo hainifanyi mimi kuwa adui wa taifa, imenifanya mimi pengine kuwa adui wa ccm na wale walionipiga risasi 16 na kutaka kuniua” Amesema Lissu.
Ameongezea kuwa kauli za Musiba si za kupuuzwa kwani zinatumika kama pazia la kuhalalisha mashambulizi kwa watu ambao wanaipinga serikali kihalali.
Hivyo amewaomba Watanzania kukabiliana na Musiba na watu wote waliopo nyuma yake, kwani anaamini kuwa kuna watu nyuma ya Musiba watu wasiojulikana waliomtuma kusema hayo aliyoyaongea.