Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameongoza mamia ya wakazi wa kata ya Mnacho, wilayani Ruangwa kwenye mazishi ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Bw. Daniel Mtawa ambaye alifariki dunia Mei 7, 2017.
Akizungumza na waombolezaji katika ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye kijiji cha Nandagala, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, amesema msiba uliowapata wana-Mnacho ni mkubwa, na akatumia fursa hiyo kuwapa pole wanafamilia na wanakijiji wenzake.
“Ndugu yetu Mtawa amemaliza safari yake na ametangulia mbele ya haki. Tuendelee kumuombea marehemu Mtawa, kila mtu kwa imani yake. Ninatoa pole kwa familia, kwa Mwenyekiti wa Halmashauri na madiwani wenzangu wote,” alisema.
Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, anatoka katika kijiji cha Nandagala, kwenye kata hiyohiyo ya Mnacho ametumia fursa hiyo kufikisha salamu za rambirambi ambazo zilitolewa na Rais, Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
“Mheshimiwa Rais ametoa salamu za pole kwa mke wa marehemu, familia na wana-Ruangwa wote. Pia Mheshimiwa Makamu wa Rais, anawapa pole wana-Ruangwa wote kwa msiba huu mzito,” aliongeza.