Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoa wa Lindi kujenga eneo la kupumzikia abiria kwenye maegesho ya kivuko katika maeneo ya Lindi na Kitunda ili wananchi wa maeneo ya Lindi na Kitunda waanze kupata huduma ya kivuko.
Majaliwa amesema hayo wakati alipotembelea na kufanya ukaguzi katika eneo la mradi wa ujenzi wa gati kwenye Manispaa ya Lindi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Lindi na kusema kwamba ameridhishwa na utekelezaji wake.
“Jengeni sehemu ya kupumzikia abiria katika pande zote mbili, upande wa Lindi na wa Kitunda. Mbali na abiria kupata eneo la kupumzikia pia itarahisisha hata ukataji wa tiketi jambo litakawarahisishia ukusanyaji wa mapato.”
Pia Majaliwa alitembelea chuo cha Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoa wa Lindi na kusema kwamba ameridhishwa na utoaji wa elimu chuoni hapo na kuwaagiza viongozi waanzishe mafunzo ya mafuta na gesi ili vijana waweze kupata ujuzi na kuajiriwa kwenye sekta hiyo.