Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amesema kuwa wakati anaanza vita ya dawa za kulevya haikuwa rahisi kwani alipata wakati mgumu na kuongeza kuwa vita hiyo haijawahi kumuacha mtu salama.
Amesema kuwa ili uweze kufanikiwa katika mapambano hayo lazima uwe na uhakika na Mungu wako ili kuwa salama na kazi hiyo ya mapambano.
Aidha, amesema kuwa waumini wote wanaoendelea kumuombea wana uhakika na Mungu, kwani watu wengi walianza kuhoji maswali mengi kuhusu njia iliyotumika kuwabaini watuhumiwa.
Vile vile, Makonda amesema vita hiyo ni ya kiroho na amewaomba waumini wa Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kimara kuendelea kumuombea ili aweze kuwakomboa vijana wengi wanao angamia na dawa za kulevya.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye alikuwa ni mmoja wa watu ambao walihudhuria ibaada hiyo alijikuta akibubujikwa na machozi baada ya kupewa nafasi ya kuwasalimia waumini wa Kanisa hilo.
Kabla ya kuanza kulia, Makonda alitumia muda wake mwingi madhabahuni kueleza nia yake ya kuendelea na mapambano ya dawa za kulevya jijini Dar es salaam.
“Sitakaa kimya wala sitaruhusu uovu ukatize katika anga la utawala niliopewa,”amesema Makonda.
Hata hivyo, amesema kuwa watu hawapaswi kulalamika wala kuhuzunika kwa watu ambao wanaongea kila siku kwenye mitandao ya kijamii, kwani hiyo ni ishara kuwa kazi inayofanyika katika ulimwengu wa roho inalipa.