Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameanza kutekeleza ahadi aliyoitoa ya kupanga mji katika muoenekano mzuri wa jiji la biashara utakaovutia wananchi wengi wa ndani na nje kuja kufanya biashara.
Makonda alitoa ahadi hiyo baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, alipofanya mkutano na wenyeviti wa serikali za mitaa, ambapo amezindua mpango mkakati wa ujenzi wa eneo moja kubwa la kufanyia biashara ya kuuza magari (used cars) pamoja na vifaa vya magari na huduma zingine zinazoendana na baishara hiyo ikiwemo utoaji wa Bima na Leseni za magari, pia huduma za kibenki, Ofisi za mamlaka ya Mapato (TRA) katika eneo moja (one car stop center).
Makonda amesema tayari Serikali ya Mkoa imeshatenga eneo kubwa na la kutosha katika manisapaa ya Kigamboni ambalo litatumiwa na wafanyabiashara wote wa magari katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo katika utekekezaji wa mpango huo, ametoa ‘offer’ ya bure kwa miaka mitatu kwa wafanyabiashara kutumia eneo hilo pasipo malipo au tozo ya kodi ya pango au kiwanja hatua itakayowawezesha kutumia unafuu huo kujenga uzio na Sehemu za ofisi katika maeneo hayo.