Mbunge wa Viti Maalumu wa chama cha mapinduzi CCM, Mkoa wa Njombe, Neema Mgaya ametoa msaada wa mashuka ya kulalia wagonjwa pamoja na mifuko ya saruji kwa ajili ya kuchangia nguvu za wananchi katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya katika wilaya hiyo.
Akizungumza mara baada ya kutoa misaada hiyo katika kituo cha afya Ludewa ‘’K’’, Lugalawa, Mlangali pamoja hospitali ya wilaya hiyo Mbunge Neema amesema ametoa misaada hiyo kutokana na kwamba Serikali kupitia chama cha mapinduzi (CCM) imejizatiti kuhakikisha inaboresha huduma za afya kwa kila kijiji zahanati na kila Kata kituo cha afya.
‘’Nimetoa mashuka zaidi ya 60 kwa wilaya hii pamoja na saruji zaidi ya tani mbili na hii yote ni kutokana na uhitaji uliopo na nitafika kila wilaya katika mkoa huu…mifuko hii ya saruji inakwenda kuunga mkono juhudi za wananchi wetu..nipo hapa kwa ajili ya kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi CCM’’ amesema Neema Mgaya
Akizungumza mara ya kupokea msaada huo mmoja wa wakazi wa Lugarawa Firomenda Haule amesema wanamshukuru mbunge huyo kwa kuunga mkono juhudi zao na kwamba wanaamini changamoto zao nyingine zitafikishwa bungeni.
‘’Tunamshukuru Mbunge Neema kwa kutuunga mkono na kwamba kama mbunge mwanamke utaendelea kufikisha changamoto zetu nyingine za kuanzisha ujenzi wa vituo vya afya’’ amesema Firomenda.
Pia, Mbunge huyo akiwa katika ziara yake hospitali ya wilaya ya Ludewa, mganga mkuu wa hospital hiyo Dkt. Nelson Kimolo amemueleza Mbunge huyo kuwa wanakabiliwa na upungufu wa madaktari akiwemo mtaalamu wa usingizi katika wodi ya upasuaji hali inayokwamisha wakazi wa wilaya hiyo kupata huduma ya upasuaji hospitalini hapo.