Baraza la Habari Tanzania (MCT) limezindua Ripoti ya hali ya Vyombo vya Habari hapa nchini kwa mwaka 2016 (State of the Media Report) ambapo ripoti hiyo hutolewa kila mwaka ili kuushirikisha umma.
Baraza hilo limetoa ripoti kuhusu kuvamiwa kwa Studio ya Clouds Media na kubaini kuwa tukio hilo liliathiri uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa wahariri.
Hayo yamesemwa mapema hii leo jijini Dar es salaam na Katibu wa Baraza hilo, Kajubi Mukajanga, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mbapo amesema kuwa ripoti hiyo haina lengo baya, bali ni kuweka bayana hali ya tasnia ya habari na kwamba jambo hilo si mara ya kwanza kwani baraza hilo limekuwa likitoa ripoti kama hizo kila mwaka.
“Hatujafanya uchunguzi huu kwa kuwa tuna mapenzi na Clouds Media wala kwa sababu tuna mahusiano na Mkuu wa Mkoa, badala yake tumetoa ripoti hii kwa mujibu wa katiba ya MCT,” amesema Mukajanga.