Viongozi wa halmashauri na majiji nchini wametakiwa kuharakisha utoaji wa vibali vya ujenzi na kuachana na urasimu unaosababisha kuwepo kwa ujenzi holela.

Agizo hilo limetolewa jijini Arusha na Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa nyumba kumi za mfano za mradi wa mji wa kisasa wa  Safari City.

Amesema kuwa kumekuwepo na ucheleweshaji mkubwa wa vibali vya ujenzi unaosababishwa na wahusika wenyewe hivyo kupelekea wananchi hao kujenga kiholela kutokana na wananchi hao kuchoka kusubiri.

Aidha kufuatia hali hiyo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kufanya ukaguzi wa mafaili ya vibali vya ujenzi ili kugundua idadi ya watu ambao hawajapatiwa vibali vyao mpaka sasa hivi.

“Unajua idadi kubwa ya wananchi wanaojenga kiholela sio kwamba wamevunja sheria bali wanafanya hivyo kwa ajili ya ucheleweshaji wa vibali kwa hiyo hatua hiyo inasababisha pia kuchelewa kutoana na kusubiri kwa muda mrefu bila kupata jibu lolote,”amesema Lukuvi.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa shirika la nyumba la taifa, Nehemia Mchechu amesema kuwa mradi huo wa kitovu cha mji wa kisasa wa safari city jijini Arusha una ukubwa wa hekari 559.4 na ni sehemu ya miji iliyopangiliwa kitaalamu na kwa kuzingatia sheria za mipango miji.

Kilomoni Awajibu Waliomsimamisha Uanachama
LIVE: Rais wa Misri awasili Tanzania