Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Mohamed Mpinga amepiga marufuku matumizi ya taa aina ya Sport Light kwani taa hizo zimekuwa zikisababisha ajali nyingi barabarani.
Amesema kuwa katika takwimu za ajali za barabarani visababishi vikubwa vimekuwa ni taa ambapo kwa mwaka 2015 ajali zilikuwa 104 na kwa mwaka 2016, ziliongezeka na kufikia ajali 123 hivyo imekuwa ikiongezeka kila siku.
Ameyasema hayo mapema hii leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mpinga amesema kuwa taa hizo hutumika vibaya hasa nyakati za usiku na kuwa chanzo cha ajali kwa kuwa zinapotumika hupotea uwezo wa mtumiaji mwingine wa barabara.
“Kutokana na ukweli kwamba matumizi yasiyo sahihi ya taa hizo imekuwa ni chanzo cha ajali, ni marufuku gari kufungwa taa za aina yoyote zenye mwanga mkali pamoja na sport light kwani hizo zimekuwa ni hatari kwa watumiaji wa barabara kwa kuwa hupoteza uwezo wa kuona wa dereva mwingine,”amesema Mpinga.
Hata hivyo, Mpinga amesisitiza kuondolewa kwa taa hizo ziwe za kutoka kiwandani au za kuongeza katika magari yote yaliyofungwa taa hizo na kuongeza kuwa kwa wale watakao kaidi agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.