Wakili wa Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Tundu Lissu, Fatma Karume amesema Polisi walikataa kumpa dhamana mteja wake jana jioni mara baada ya kukamatwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere International JNIA.
Ameyasema hayo mapema hii leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, ambapo amesema kuwa baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Kati Lissu alitakiwa kuandika maelezo na kupewa onyo kwa kosa la uchochezi lakini baada ya kufanya hivyo Polisi waliendelea kumshikilia.
“Lakini cha ajabu mpaka sasa hivi hatujaambiwa Lissu kamchochea nani, kosa la uchochezi lazima lilete madhara au uhalifu kwa wengine na ni lazima liwe la uhalifu.” amesema Wakili Karume.
Hata hivyo, ameongeza kuwa wataiandikia barua mahakama ili iweze kuliamuru Jeshi la Polisi kumpeleka Tundu Lissu makamani ili hatua zingine za kisheria ziweze kuchukuliwa na ikiwa pamoja na kufunguliwa mashtaka.