Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limesema kuwa milipuko iliyotumika kulipua Ofisi za IMMMA Advocates zilizopo jijini Dar esalaam ilikuwa ni milipuko iliyotengenezwa kienyeji na si kama inavyosemekana kuwa ni mabomu.
Hayo yamesemwa Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaa, Kamanda Benedicto Kitalika alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hii leo, ambapo amesema kuwa milipuko iliyotumika kulipua ofisi hizo ni ya kienyeji.
“Nipende kuchukua nafasi hii kutoa taarifa ya uchunguzi wa awali kuhusu mlipuko uliotokea katika ofisi za IMMMA Advocates, ni kwamba milipuko iliyotumika ilikuwa ni ya kienyeji hivyo niwaombe waathirika kuwa na moyo wa subira wakati jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi,”amesema Kitalika.
Hata hivyo, Kitalika amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo katika shughuli zake za amani ili liweze kuimarisha hali ya usalama katika maeneo yote ya jiji la Dar es salaam.