Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema ingekuwa masharti yanalegezwa angemuomba Askofu Mkuu, Gervas Nyaisonga akawe Padri ili aweze kulihubiri na kulitangaza neno la Mungu ambalo ni la muhimu katika maisha yetu hapa duniani.
Rais Magufuli amesema hayo leo Aprili 28, 2019 katika misa ya kumsimika Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya iliyofanyika katika Viwanja vya Sokoine na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Amesema kuwa wakati anakua alitamani kuwa Askofu au Padri lakini kwa bahati mbaya alishindwa kuwa Katekista wala Mwenyekiti wa Jumuiya.
“Hata waimbaji walipokuwa wakiimba wamenikumbusha wakati ule nikawa najiuliza nilikosea wapi, yangekuwa masharti yanalegezwa ningemuomba baba Askofu Mwaisonga nikawe Padri ili niweze kulihubiri na kulitangaza neno la Mungu ambalo ni la muhimu katika maisha yetu hapa duniani,” amesema Rais Magufuli.
Amesema inawapasa watu kufahamu ni kwa namna gani kazi hiyo inahitaji mkono wa Mungu katika kuitekeleza.
Rais Magufuli ameongeza kuwa Askofu ni daraja takatifu na wito kutoka kwa Mungu hivyo ni kazi ngumu yenye changamoto zake huku akitolea mfano wa maandiko katika Biblia kutoka kitabu cha waraka wa mtume Paulo kwa Tito sura ya 1 mstari wa 7 hadi wa 9.