Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amezungumzia uhusiano wa kikazi kati yake na Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi akimtaka waungane katika kuuendeleza mkoa huo.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24 hivi karibuni, Chalamila alitoa mtazamo wake kuhusu madai ya kuwepo kwa mgongano kati ya Mhimili wa Serikali na Mhimili wa Bunge, ambapo alieleza jinsi mihimii hiyo inavyopaswa kufanya kazi kwa kushirikiana.
Akitoa mfano wa Sugu ambaye ni mbunge na yeye ambaye anaiwakilisha Serikali, alieleza kuwa wanapaswa kuweka kando itikadi za vyama vyao na kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wa Mbeya.
“Mimi ninachoamini ni kwamba mimi na ndugu yangu mbunge tunajenga nchi moja, sikusudii na sitambui kwamba tunagawana watu, na sitarajii kama hatambui kama Mheshimiwa Magufuli ni Rais wa Tanzania,” Chalamila ameiambia Dar24.
“Kwahiyo mimi natambua kwamba miongoni mwa watu ambao mimi nawaongoza katika Mkoa wa Mbeya ni pamoja na yeye pia. Kwahiyo tunapaswa tushirikiane, tuwe wamoja na inapaswa tusiweke hisia za vyama vyetu mbele, inapaswa tuweke maslahi ya Watanzania mbele na inapaswa tuone ni jinsi gani nchi inaenda mbele na Mbeya itakuwa kwa kiasi gani,” aliongeza.
Oktoba mwaka jana, katika mkutano wake na wafanyabiashara wa Soko la Soweto mkoani humo, Mkuu huyo wa Mkoa alikanusha tetesi kuwa amepelekwa mkoani humo kwa lengo la kumng’oa Sugu.
Alisema kuwa Sugu ni mali ya wananchi aliyechaguliwa kwa kura, hivyo hakuna nia ya kumuondoa kwa njia tofauti.