Shirika la Serikali la Maendeleo la Taifa (NDC), limeingia ubia na Kampuni binafsi ya EDOSAMA Hardware ambao ni wafanyabiashara na watafiti wa mazao ya misitu hapa nchini, kwa pamoja wanatarajia kuanzisha kiwanda kikubwa na cha kwanza nchini kwa uzalishaji wa samani kwa kutumia mabaki ya miti maarufu kama NDF.
Hatua hiyo ni kufuatia utafiti uliofanywa na EDOSAMA Hardware na kugundua kwamba viwanda vingi vya mbao nchini hutumia asilimia 30 tu ya zao la miti huku mabaki yakiwa yanatupwa, hivyo wameamua kuanzisha kiwanda hiko kitakacho hakikisha zao la mti hapa nchini linatumika kwa asilimia 100.
Lakini pia amesema nchini Tanzania wanatumia sana bidhaa za samani zinazotengenezwa kwa mabaki ya mti kutoka China hivyo wamekuja na mpango mkakati ambapo wanatarajia kujenga zaidi ya viwanda 300 vya samani Jijini Dar es salaam, huku viwanda 100 kujengwa Dodoma na vingine 100 kujengwa Mwanza.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa EDOSAMA Hardware, Edward Maduhu katika banda la Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) pindi walipotembelewa na Dar24 Media katika msimu huu wa maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya sabasaba jijini Dar es salaam
Kufuatia ujenzi wa viwanda hivyo ajira nyingi zinatarajiwa kutolewa viwandani hapo lakini pia kuongeza pato la taifa.
Tazama hapa chini namna ambavyo viwanda hivyo vitafanya kazi ya uchakataji mabaki ya miti na kutengeneza samani.