Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa Taifa unaridhisha, ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 5.7.
Majaliwa amesema hayo wakati akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge, mjini Dodoma Novemba 17, 2017.
“Mwenendo wa uchumi wetu ni wa kuridhisha, mfano, ukuaji wa uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 5.7, robo ya pili ilikuwa asilimia 7.8 na nusu ya kwanza ya mwaka huu ilikuwa ni asilimia 6.8.”
Majaliwa amesema hali hiyo inafuatia kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na usimamizi thabiti wa matumizi ya Serikali, ambapo nakisi ya bajeti ya Serikali imeshuka na kufikia asilimia 1.9 kwa mwaka 2016/2017
Pia amesema akiba ya fedha za kigeni inatosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa zaidi ya kipindi cha miezi mitano, ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi minne.
Akizungumzia kuhusu kasi ya upandaji bei, Waziri Mkuu amesema takwimu zinaonyesha kwamba katika nusu ya mwaka 2017, mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika kiwango cha tarakimu moja.
“Takwimu zinaonyesha kwamba mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Oktoba 2017 ulikuwa ni asilimia 5.1 ikilinganishwa na asilima 5.3 mwezi Septemba, 2017.”
Amesema kupungua kwa mfumuko wa bei kumechangiwa na kupungua kwa bei wa bidhaa za vyakula, ambavyo vimepungua kutoka wastani wa asilimia 9.3 mwezi Septemba, 2017 hadi asilimia 8.8 mwezi Oktoba, 2017.