Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameupongeza uongozi wa Shirika la Nyumba (NHC) kwa kukamilisha ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mnolela mkoani Lindi kwa muda mfupi.
Majaliwa ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mnolela baada ya kuzindua zahanati hiyo iliyosimamiwa na NHC.
Amesema ujenzi wa zahanati hiyo ya kisasa mwezi Machi, 2017 na sasa tayari kimekamilika, jambo ambalo litarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa eneo hilo na wa jirani.
“Rais wetu Dkt. John Magufuli amedhamiria kuwaondolea wananchi changamoto za mbalimbali zikiwemo za huduma za afya, hivyo tuendelee kumuunga mkono.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa NHC, Bw. Nehemia Mchechu alisema mradi wa ujenzi wa zahanati hiyo ulisimamiwa na NHC na umegharimu sh. milioni 65.5.
“Shilingi milioni 15 zilitolewa na Rais. Dkt. Magufuli, sh. milioni 10 zilitolewa na Mheshimiwa Mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye, NHC ilitoa sh. milioni 10 na kiasi kilichosalia ni mchango wa halmashauri.”
Awali Mbunge wa jimbo la Mtama, Mheshimiwa Nape alimshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa mchango mkubwa alioutoa katika mradi wa ujenzi wa zahanati hiyo.
Nape alisema zahanati hiyo ni mkombozi kwa wakati wa kijiji cha Mnolela na wananchi wengine wanaoishi kwenye maeneo yaliyo jirani na kijiji hicho.