Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Francis Zuakuu kumkamata aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Bulagamilwa, Ntemi James kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa sh. milioni 141 za kijiji hicho.
Ametoa agizo hilo leo Agosti 16, 2018 wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Igunga, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Tabora.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali kumuomba awasaidie katika kulipatia ufumbuzi suala hilo la upotevu wa fedha za kijiji kwa kuwa ni la muda mrefu na hakuna hatua zilizochukuliwa.
Kutokana na malalamiko hayo Waziri Mkuu amemtaka kamanda wa TAKUKURU wa wilaya hiyo ahakikishe anawatafuta watu wote waliohusika na upotevu wa fedha hizo za kijiji akiwemo na alitekuwa mtendaji wa kijiji cha Bulagamilwa, ambaye kwa sasa ni Mtendaji wa kata ya Igurubi.