Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi kuanzia leo, kufuatia wimbi kubwa la usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi bila kibali.
Amesema kuwa kuanzia leo, yeyote atakayekamatwa akitorosha chakula kwenda nje ya nchi, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na gari lake tutalitaifisha na litaishia Jeshi la Polisi.
Majaliwa ametoa agizo hilo leo Juni 26, 2017 wakati akitoa nasaha kwenye Baraza la Eid lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Eid.
“Kuanzia leo, ni marufuku kwa mtu yoyote kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali. Serikali inahamasisha uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda nchini. Kama tutatoa vibali, ni lazima mtu alazimike kusaga nafaka ili kutoa ajira nchini,” amesema.
“Mimi nasema kuanzia leo, yeyote atakayekamatwa akitorosha chakula kwenda nje ya nchi, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na gari lake tutalitaifisha na litaishia Jeshi la Polisi. Tunafanya hayo kwa lengo la kuwalinda Watanzania tusikumbwe na baa la njaa.”