Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni, na Michezo, Prof. Harrison Mwakyembe amesema kuwa anamshangaa Mbunge wa Jimbo la Chemba Mkoani Dodoma, Juma Nkamia kuhoji uwepo wake katika mkutano wa mwanamuziki wa bongofleva ‘Roma’ na waandishi wa habari uliofanyika juzi Jijini Dar es salaam.
Mwakyembe amesema kuwa yeye ni Waziri mwenye dhamana ya Sanaa, hivyo ni haki yake kuwepo katika mkutano huo wa msanii ‘Roma’ na waandishi wa habari kwakuwa ulifanyikia Habari Maelezo ambayo iko chini ya Wizara ya Habari.
“Kukutana na Wasanii sio dhambi kwa sababu mimi ndiye mlezi wao, nilikutana na Ney ofisini kwangu hapa Dodoma, hata Roma naye kule Dar es salaam, Habari Maelezo ni Ofisini kwangu, ulitaka ukutane nao wewe? au ulitaka nikutane naye mgahawani,”amesema Mwakyembe.
Ameyasema hayo mapema hii leo Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge, amesema kuwa hilo ni suala dogo tu la uelewa ambalo, Juma Nkamia hakutakiwa kushangaa na kuumiza kichwa.
Hata hivyo, katika hatua nyingine Mwakyembe amesema kuwa Serikali ina mpango wa kuanzisha mfumo wa lugha za ishara katika vituo vya televisheni ambapo amesema hawezi kuanza kuvibana vituo binafsi mpaka atakapokamilisha mfumo huo katika televisheni ya taifa TBC.