Mgombea urais kupitia Chama cha wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amezindua kampeni za chama hicho katika uwanja wa Sabasaba mkoani Mtwara .
Akizindua kampeni hizo, Lipumba ametaja mambo ambayo yatapewa kipaumbele katika serikali yake iwapo atafanikiwa kuwa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania. Miongoni mwa mambo ambayo chama hicho kitayapa kipaumbele ni pamija na:
Kuboresha sekta ya uvuvi na uchumi wa baharini, kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika kwa asilimia kubwa zaidi. Hii ni pamoja na kuongeza uwezo wa uvuaji samaki na upatikanaji wa soko la bidhaa hizo.
CUF imesema itaboresha kilimo kwa kuwekeza zaidi kwenye nafaka kwani tayari India imeihakikishia Tanzania soko la uhakika la nafaka zitakazolimwa nchini na kuhakikisha soko la uhakika la korosho ambayo imekuwa ikiingiza fedha za kigeni.
“Kanda ya Kusini imajaliwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwamo korosho, kahawa, pamba, katani chai, tumbaku na gesi, lakini hainufaiki na rasiliamali hizi, mkinichagua kuwa rais nitahakikisha ninainua uchumi wa mikoa hii kupitia fursa zilizopo,” amesema Profesa Lipumba.
Chama hicho pia kimeahidi kuhakikisha wakazi wa mikoa ya kusini mwa Tanzania wananufaika na mradi wa gesi na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na katiba mpya.
Aidha, Lipumba imesema itahakikisha elimu bora kwa watoto wote na kwamba kila mtoto atasoma kadiri ya uwezo wa akili yake na sio uwezo wa fedha za mzazi wake huku wakiahidi wanafunzi kuanza kutumia kompyuta.
Kama ambavyo imekuwa kwa wagombea wengine, sekta ya afya pia imekuwa miongoni mwa vipaumbele vya chama hicho ambapo, kimeahidi kuboresha huduma za afya kwa wajawazito na watoto kwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na akiba ya damu ya kutosha, lishe bora kwa watoto pamoja na matumizi ya teknolojia kutoa ushauri wa kitabibu kwa wagonjwa hata wale walio mbali na hospitali.