Wakati takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinakadiria watu zaidi ya 3,400 hupoteza maisha kila siku kwa ajali za barabarani, Jeshi la Polisi nchini limesema kwa mwaka 2020 limefanikiwa kupunguza ajali kwa asilimia 33.
Akizungumza, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi CP Liberatus Sabas, amesema katika kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka 2019 ajali zilizosababisha vifo ni 1,117 huku waliopoteza maisha 1,329 na majeruhi ni 2,717.
Amesema Januari hadi Novemba mwaka huu wa 2020, jumla ya matukio ya ajali ni 1,800, kati ya hizo ajali zilizosababisha vifo ni 935, waliofariki ni 1,158 na majeruhi ni 2,089.
Kamanda Sabas ameeleza hayo wakati akitoa taarifa yake ya matukio kwa mwaka 2020 kwa vyombo vya habari ambapo ambapo ajali imetajwa kuwa chanzo namba mbili cha mauaji huku wivu wa mapenzi ukiongoza kwa kusababisha mauaji nchini kwa mwaka 2020.
Aidha Sabas amesema pia kumekuwa na wimbi kubwa la wanafunzi kuacha masomo na kujiunga na makundi ya kihalifu kama lile lililokuwa kibiti mkoani Pwani na kuwataka wazazi na walezi kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wao.
“Wanafunzi waliokamatwa ni wawili bado tunaendelea kuwahoji, ni wanafunzi wa skondari. Matukio haya yamekuwa yakijirudia , hata pale Arusha wapo wanafunzi walioacha chuo kimoja cha ufundi na wakawa wanelekea Somalia, kwa hiyo ni vizuri wazazi wakakaa karibu na watoto wao kwa sababu mwisho wa siku wanasema watoto wamepotea kumbe wameenda kwenye mambo ya uhalifu,”amesema Sabas.