Idadi ya vifo vinavyosababishwa na covid-19 imevuka 200,000 nchini Marekani, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali ya nchi hiyo jana, Septemba 22, 2020.
Marekani imeshangazwa na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaopoteza maisha kutokana na virusi hivyo ingawa inaamini ndiyo nchi iliyojiimarisha zaidi katika huduma ya afya.
“Inashangaza sana na haikutarajiwa kuwa tumefikia katika hatua hii,” Reuters imemkariri mtafiti mbobezi kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.
Marekani ina visa zaidi ya milioni 6.92, vifo 201,000 na hakuna mgonjwa aliyeripotiwa kupona hadi sasa.
Hata hivyo, mtaalam huyo ameeleza kuwa huenda idadi ya vifo vitokanavyo na covid-19 nchini Marekani ikawa kubwa zaidi ya iliyoripotiwa kwakuwa baadhi ya vifo vilikuwa vinahusishwa na magonjwa mengine hususan katika kipindi cha awali cha mlipuko wa virusi hivyo.
Idadi hiyo ya vifo vitokanavyo na virusi hivyo ni saw ana athari ya vifo vitokanavyo na shambulizi la kigaidi la Septemba 11, 2001 lililofanywa na kundi la Al-Qaeda lingefanyika kwa siku 67 mfululizo kwa athari ileile.
Septemba 11 ambayo ni moja kati ya matukio mabaya zaidi kuwahi kusababisha vifo vingi ndani ya Marekani kwa siku moja ilisababisha vifo vya takribani watu 3,000, huku idadi ya waliokufa kwa covid-19 ikiwa 201,000 hadi kufikia jana.
Marekani ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa idadi kubwa zaidi ya vifo vitokanavyo na covid-19 ikifuatiwa na Brazil yenye vifo 136,895.
Tangu Covid-19 ilipobainika Desemba 2019, imesababisha vifo vya watu zaidi ya 967,000 duniani kote na visa zaidi ya Milioni 31.5.