Vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Malaria nchini vimepungua kwa zaidi ya asilimia 75 kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi huku idadi ya watu wanaougua ugonjwa huo na maambukizi mapya ikipungua kwa zaidi ya asilimia 67.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Dkt. Leonard Subi wakati wa kikao kazi cha kanda kilichofanyika jijini Dodoma.
amesema lengo la mkutano huo ni kutathmini utekelezaji wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria (NMCP), na kwamba wamedhamiria kufanikisha lengo kwa asilimia zote.
“Tumedhamiria kuondoa kabisa ugonjwa wa Malaria Tanzania na tayari mafanikio yameanza kuonekana kwani vifo vitokananvyo na ugonjwa wa Malaria nchini vimepungua kwa zaidi ya asilimia 75 kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi,” amefafanua Dkt. Subi.
Ameongeza kuwa hata maambukizi ya ugonjwa wa maralia tayari yameonesha kupungua kwani mwaka 2010 kiwango cha Malaria nchini kilikuwa ni asilimia 18 lakini kwasasa kiwango hicho kimeshuka na kufikia asilimia 7.3 kitu kinachoonesha mafanikio.
Aidha Dkt. Subi amebainisha kuwa Tanzania hivi sasa inatakiwa kuwa na mpango endelevu wa kuondoa Malaria ambao utasaidia kuondosha ugonjwa huo kwa kuangamiza mazalia yake ikiwemo viluilui pamoja na mbu wapevu.
“Hawa mbu tukipambana nao kuwaondosha tutaweza kuiondoa Malaria nchini kwani tunayo fursa kwa kutumia kiwanda chetu cha kibaha ambacho kinazalisha viuadudu hivyo tutaendelea kusambaza viadudu kwenye ngazi za Halmashauri pamoja na kutumia njia ya jamii kwa kila mtaa na vijiji,” amefafanua Dkt. Subi.
Hata hivyo ameitaka mikoa kuhakikisha inatenga fedha kwa ajili ya udhibiti wa mbu na wadudu wadhurifu kwa kuzingatia miongozo ya Wizara katika kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini.
Kikao hicho kimejumuisha waganga wakuu kutoka katika mikoa mbalimbali, wilaya, wafamasia na waratibu wa malaria wa kanda tano za mikoa ya Dodoma, Singida, Njombe, Iringa na Morogoro.