Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, imepanga kukifanyia maboresho makubwa kikosi chao kwa kusajili wachezaji wa kigeni wenye ubora na Rekodi nzuri ya kuzifikisha timu zao katika hatua nzuri za michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Simba SC imeishia hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kutolewa na Mabingwa watetezi Wydad Casablanca ya nchini Morocco kwa njia ya hatua ya penalti.
Timu hiyo, hivi kwa sasa imerejesha nguvu na akili zake katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’kwa kuhakikisha wanawapoka Young Africans mataji hayo yote, ikishindikana moja kati ya hayo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema wanafahamu walipokosea na wamejifunza, kikubwa watarejea kivingine katika msimu ujao watakapocheza michuano hiyo mikubwa Afrika kwa lengo la kucheza fainali.
Ally amesema usajili huo utamuhusisha Kocha Mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ raia wa Brazil na Bodi ya Wakurugenzi ambayo itakuwa ya mwisho ya kuwezesha upatikanaji wa wachezaji watakaopendekezwa.
“Wapo baadhi ya wachezaji ambao Kocha Robertinho hatawaacha kutokana na kuvutiwa na viwango vyao katika michuano ya kimataifa wakicheza safu ya ushambuliaji ambao ni Baleke (Jean) na Kibu (Denis) atakaowatafutia wasaidizi wao.
“Uongozi umewapitisha wachezaji hao, lakini tumepanga kukifanyia maboresho makubwa kikosi chetu kwa kuwaacha baadhi ya wachezaji ambao hawana mchango katika timu na kuingiza maingizo mapya ya usajili wa wachezaji wa kigeni na wazawa.”
“Tunahitaji wachezaji wenye ubora na kigezo tutakachokiangalia ni awe ameifikisha timu yake katika hatua nzuri ya michuano ya kimataifa Afrika msimu huu na uzuri ni kwamba kocha na viongozi wanafuatilia michuano hiyo tangu hatua ya makundi kwa kuangalia wachezaji watakaowasajili,” amesema Ally.