Vijana saba wamefariki dunia papo hapo katika kijiji cha Mavuji, Wilaya ya Kilwa baada ya ajali mbaya kutokea ambapo gari dogo aina ya Hiace kugongana uso kwa uso na lori la kampuni ya Dangote.

Inaelezwa kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa gari ndogo kushindwa kulimudu vizuri gari yake wakati akikwepa shimo.

Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi Foka Dinya, amesema kutokana na ajali hiyo miili miwili ndiyo imeweza kutambuliwa kwa majina, kutokana na vitambulisho vilivyokutwa kwenye mifuko yao.

Waliotambulika ni dereva Jerome Goefrey Kileo pamoja na Christopher Kitigo.

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, leo Machi 4, 2020, Kamanda Dinya amesema kuwa vijana hao saba walikuwa wakielekea wilayani Luangwa katika biashara zao, kwani walikuwa wamefungua mradi wa kutengeneza samani za ndani.

“Chanzo cha ajali ni mwendokasi wa gari ndogo, na walikuwa ni wafanyabiashara wana mradi wao wa kutengeneza Furniture Luangwa, miili yote saba imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, wawili vitambulisho vyao vilikutwa kwenye mifuko yao ya suruali ndio wameweza kufahamika, watano bado hawajafahamika” amesema Kamanda Dinya.

Ajali hiyo imetokea jana Machi 3, 2020, majira ya 12:00 Alfajiri.

Dkt Ndumbaro akutana na Maseneta kutoka Ufaransa
Bei ya vyakula yapaa ujenzi ukiendelea