Vijana mkoani Rukwa wametakiwa kuchangamkia tenda za serikali na kujivunia mabilioni ya fedha yanayotolewa kwa ajili yao ambayo ni zaidi ya Shilingi Bilioni 900. 

Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma, PPRA, Joseph Muhozi, amesema Katika bajeti ya serikali ya kila mwaka inayopitishwa Bungeni, zaidi ya 70% inapelekwa kwenye ununuzi wa Umma, ambapo kwa mwaka huu ni zaidi ya trilioni 30.

Kupitia Kipindi cha Clouds 360, PPRA ilishiriki mjadala maalumu ambao ulihusisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga na wakuu wa wilaya wa mkoa huo wakiwa na lengo la kubainisha fursa za kibiashara zinazopatikana katika mkoa huo, pamoja na jinsi ya kufanya biashara na Serikali.

“Sheria ya Ununuzi wa Umma, inampatia nafasi kijana ambapo katika taasisi zote za serikali ni lazima kutenga asilimia 30 kwa ajili ya makundi Maalumu ambapo vijana wapo ndani yake, na asilimia za vijana ni 10 ya Trilioni 9 ambayo ni zaidi ya Bilioni Mia 9,” amesema Muhozi.

Ameongeza kuwa ili Kijana aweze kupata pesa hizi anatakiwa kujiunga na Kikundi ambacho kitahusisha vijana kuanzia 5 hadi 20, na wasajiliwe Halmashauri wawe na vitambulisho vya Nida, na TIN kutoka TRA, na baadae watume Jina la kikundi PPRA kwa kusema kuwa wanataka kujihusisha na tenda za Serikali.

“Kuna Mfumo ambao kila mtu anayeomba tenda za serikali, anajisalili humo na kurahisisha upatikanaji wa Tenda. Mfumo huo ni www.taneps.go.tz hivyo akishajisajili kwa hitaji lake atapata taarifa kila wakati itakapotangazwa tenda inayohusisha kazi yake na hakuna mtu anaejua maombi hayo isipokuwa yeye mwenyewe na mfumo huo,” amesema Muhozi.

Muhozi ameongeza kuwa Uchaguaji wa watu wanaopewa tenda hizo hufanyika kwa uwazi na vigezo vyote hufuatwa hivyo kama muombaji wa tenda hajachaguliwa ni lazima apewe sababu za kutochaguliwa na kama hajaridhika anaweza kukata rufaa kwa kutaja sababu za kutoridhika.

“Unaandika barua kwa Mkuu wa taasisi husika, na anatakiwa kukujibu kwa siku 7, asipokujibu au usiporidhika unakata rufaa tena kwa mamlaka ya Rufani ya zabuni, kama bado hujaridhika na maamuzi unakwenda mahakama kuu,” ameongeza Muhozi.

Muhozi ameongeza kuwa, “PPRA tumeamua kudandia hili basi la Fiesta ili kuwafutia vijana wote na kuwapa elimu hii ya upatikanaji wa hizi pesa zao, pia tuna Mafunzo ambayo huwa tunatoa kwa kuzunguka nchi nzima ingawa changamoto kubwa ni muitikio.”

Mkoa wa Rukwa unatajwa kwa fursa nyingi kwa vijana ambapo katika Manispaa hiyo kuna zaidi ya bilioni 15 ambazo zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa umma, na 10% yake ni ya vijana.

PPRA ni moja kati ya washirika wa Tamasha la Fiesta la Clouds TV ambapo katika awamu hii tamasha hilo linaanzia mkoani Rukwa wilaya ya Sumbawanga.

Ubunifu na utafiti suluhisho kwa serikali mtandao
TPLB yasogeza mbele mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara