Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) itacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya wenyeji wa fainali za Afrika kwa vijana 2017, timu ya taifa ya Gabon mwishoni mwa mwezi huu nchini Morocco.
Shirikisho la soka nchini (TFF), limethibitisha taarifa za mchezo huo ambao haukuwepo kwenye mpango wa maandalizi ya timu ya Serengeti Boys unaoendelea mjini Rabat nchini Morocco tangu juma lililopita.
Afisa habari wa TFF, Alfred Lucas amezungumza na Dar24 na kueleza kuwa, Gabon wameomba kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Serengeti Boys, ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na fainali za vijana ambazo zitaanza rasmi Mei 14 hadi 28. mwaka huu.
“Tunashukuru kupata mchezo huu wa kirafiki kwa ajili ya timu yetu, na tayari Gabon wamekubaliana na sisi kuhusu tarehe ya kuchezwa kwa mchezo huu, tutacheza nao Aprili 22 na 25,” alisema.
“Tayari tumeshatoa taarifa CAF na FIFA kuhusu michezo hiyo ambayo ni lazima iingizwe kwenye rekodi angalau ya mwezi wa huu wa nne, ambapo matokeo yake yatakua yanafanya tathmini ya nafasi yetu ya viwango vya ubora wa soka dunia.
“Gabon ni moja ya timu mahiri kwa sababu ndio wenyeji wa fainali za vijana kwa mwaka huu, lakini jingine ni timu ya tatu kutaka kucheza na Tanzania kutoka kundi A, tumeshacheza na Ghana, tutacheza na Gabon na baadae tutacheza na Cameroon mapema mwezi wa tano, Alfred lucas ameiambia Dar24.
Kuhusu kambi ya Serengeti Boys Alfred amesema inaendelea vizuri na mpaka sasa hawajapokea taarifa zozote ambazo zinakwenda kinyume na matarajio yao.
Katika fainali za vijana chini ya umri wa miaka 17 za Afrika 2017, Serengeti boys imepangwa kundi B sanjari na Niger, Mali na Angola.