Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro imemfikisha mahakamani Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) mkoani humo, Gresta Sodoka kwa tuhuma za kugushi vyeti.

Katika kesi hiyo, Sodoka ambaye aliwahi kuwa diwani wa viti maalum (CCM) katika Manispaa ya Moshi anadaiwa kugushi cheti cha kitato cha nne, na cheti cha shahada ya kwanza ya Sayansi ya Uuguzi kutoka Chuo Kikuu cha Texas nchini Marekani.

Mshitakiwa huyo alisomewa mashtaka manne mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Moshi, Anthony Ngowi.

Kwa mujibu wa Mwananchi, pamoja na mashtaka mengine, Sodoka alidaiwa kuwa katika siku isiyojulikana kabla ya Machi 24 mwaka 1978 akiwa mjini Moshi aligushi cheti cha kumaliza kidato cha nne chenye namba zinazoonekana kuwa zimetolewa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Kadhalika, ilidaiwa kuwa Septemba 11 mwaka 2009 akiwa mjini humo, aligushi karatasi la matokeo (transcript) ya Chuo cha Texas Women kilichoko nchini Marekani, kikionesha kuwa alikuwa mwanafunzi wa chuo hicho kikiwa na namba za utambulisho za kugushi.

Sodoka pia anadaiwa kugushi cheti cha shahada ya kwanza ya uuguzi kikionesha kuwa kilitolea na Chuo Kikuu cha Texas cha nchini Marekani na kwamba vyeti vyote alivitumia katika kujipatia kazi ya uuguzi ambayo alistaafu mwaka jana akiwa na cheo cha muuguzi mwandamizi wa Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Hata hivyo, mshtakiwa aliyakana mashtaka yote na kuachiwa baada ya kukidhi masharti ya dhamana. Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Mei 12. Takukuru ilieleza kuwa bado upelelezi haujakamilika.

Thomas Ulimwengu Kusota Benchi Kwa Miezi Mitatu
Vijana Wa Gabon Kuipima Serengeti Boys