Vijana waliopata fursa za ajira nje ya nchi wameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuja na njia bora za kuratibu na kusimamia watu wanaoajiriwa nje ya nchi kwa lengo la kulinda haki za watanzania.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa zoezi la kuwaaga vijana 50 ambao wamepata fursa za ajira nchini Saudi Arabia kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira (TaESA) kwa kushirikiana na kampuni ya wakala wa ajira Bravo Job Center Agency.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Nganga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Bravo Job Center Agency na Vijana waliopata fursa za ajira nchi ya Saudi Arabia mara baada ya kuwaaga katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mmoja wa wanufaika, Exaver Jauri amesema kumekuwa na dhana potofu hususan zinapotokea fursa za ajira nje ya nchi na kuwashauri vijana kuacha kuwa na mitazamo potofu kwa kuwa serikali kupitia TaESA imekuwa ikiratibu na kusimamia ajira za watanzania nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ajira Joseph Nganga amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia TaESA imeendelea kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri ndani na nje ya nchi pamoja na kusimamia michakato yote ya watu wanaoenda kufanya kazi nje ya nchi.