Uwepo wa uhaba wa kifaa cha uchunguzi wa Virusi Vya UKIMWI (HIV Kits), katika vituo vya afya vya Serikali Zanzibar, umepelekea huduma ya upimaji wa maradhi hayo kuwa hafifu kiasi cha kupelekea Vijana ambao wameonesha mwamko wa kutaka kupima na kujua Afya zao kukosa huduma hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara iliyofanywa na Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA-ZNZ, watoa huduma za Afya katika vituo mbalimbali vya Wilaya ya Magharibi “B” na Wilaya ya Kati Unguja, wamesema jambo hili pia limeathiri jamii.
Wataalamu hao kutoka kituo cha afya Fuoni, Tunguu, SUZA, Mwera, Magirisi pia waliwaeleza Wananchi hasa vijana kuwa wamehamasika kupima VVU na hufika kwa wingi kupata huduma hiyo, lakini kutokana na uhaba wa kifaa hicho huduma hiyo haipatikani kwa sasa.
Daktari Kiongozi wa Kituo cha Afya Fuoni, Sultani Shela alisema tatizo hilo lina zaidi ya miezi miwili na vifaa havipatikani katika vituo vya huduma rafiki kwa vijana pamoja na vituo vya afya, hali ambayo wateja hulazimika kwenda Hospitali binafsi ambapo huduma hiyo hutolewa kwa malipo.
Alisema, huduma hiyo hupatikana kwa wajawazito pekee ambao hulazimika kujua afya zao ili kumkinga mtoto na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI, huku Khadija Ali Khamis wa kituo cha huduma rafiki kwa vijana Mwera akidai Vituo vyote vya Serikali huduma ya upimaji wa VVU ni bure na Wananchi hufika kwa wingi ili kujua afya zao.
Aidha, Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, alikiri uwepo wa uhaba wa kifaa hicho kutokana na kuchelewa kwa kontena lenye vifaa toka nje ya nchi na kwamba kuanzia Septemba 4, vifaa hivyo vitaanza kusambazwa katika vituo vyote vya afya vya Serikali, ili kuendelea kutoa huduma ya uchunguzi wa VVU.
Hata hivyo, Waziri huyo aliwataka Wananchi kuendelea kuvitumia vituo vya afya na vituo vya huduma rafiki kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za kiafya, ikiwemo uchunguzi wa VVU ambapo maambukizi yake kwa sasa yapo katika makundi maalum ikiwemo vijana wanaotumia dawa za kulevya na wanaofanya biashara ya ngono.
Ziara hiyo ya Waandishi wa Habari, imeandaliwa na Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA-ZNZ, kupitia mradi wa kuendeleza utetezi wa afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana mjini na vijijini ambao unaendeshwa katika Wilaya mbili za Unguja ya Kati na Magharibi “B” na wilaya ya Chakechake kwa Pemba kwa ufadhili wa Wellspring Philanthropic Fund – WPF, toka nchini Marekani.