Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Brazil Vinicius Junior amemwagia sifa Carlo Ancelotti kama kocha bora zaidi duniani baada ya Real Madrid kushinda mabao 2-0 dhidi ya Chelsea.
Real Madrid inayotetea taji la Barani Ulaya, ilichomoza na ushindi huo katika mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa usiku wa kuamkia Alhamis (April 13).
Ancelotti, ambaye amekuwa akihusishwa mara kwa mara kuchukua kazi iliyoachwa wazi ya timu ya taifa ya Brazil msimu huu, ana mkataba wa Madrid hadi mwaka 2024.
Amepata shinikizo baada ya kuwa nyuma kwa alama 13 dhidi ya FC Barcelona katika mbio za kuwania taji la LaLiga msimu huu 2022/23, licha ya kuiongoza Madrid kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa na Fainali ya Copa del Rey.
“Hebu tumaini ni wote wawili!” Vinicius alisema, akicheka, alipoulizwa na waandishi wa habari kama angependelea kumuona Ancelotti akiwa kocha wa Madrid au Brazil.
“Kwangu mimi, ndiyo yeye ni kocha bora zaidi duniani. Sijui kuhusu kila mtu, lakini kwangu na kwa wachezaji wa hapa, yuko.”
Vinicius amechangia katika kufunga mabao 20 katika mechi 20 zilizopita za Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiwa amefunga mabao 10 na asisti 10, likiwemo la mshindi katika Fainali ya mwaka jana.