Licha ya makubaliano, ya kusitisha mapigano kati ya makundi hasimu baada ya kutokea kwa ghasia wiki chache zilizopita, mapigano mapya yameibuka katika jimbo la kusini mwa Sudan na kusababisha vifo vya watu saba ambapo Wananchi wamesema Viongozi hawawatendei haki na wanawatesa.
Taarifa za vyombo vya usalama, katika jimbo la Blue Nile imesema mapigano hayo mapya ya kikabila ambayo pia yameacha majeraha na vilio kwa raia, yameanza tena eneo hilo bila sababu zozote za wazi, licha ya juhudi za dhati za serikali kuimarissha usalama na kukomesha uhasama.
Mapigano hayo, yalisababisha vifo vya watu saba na wengine 23 kujeruhiwa baada ya pande mbili hasimu kushambuliana hasa katika eneo la Kijiji cha East Ganis na eneo la Roseires ambapo Wananchi hao wanasema hawaoni jitihada za utafutaji wa suluhu ya kudumu.
Julai 2022, mapigano katika eneo hilo yalishindanisha makabila ya Hausa dhidi ya jamii hasimu, ikiwa ni pamoja na watu wa Berta na kuacha watu wasiopungua 105 wakiuawa na kadhaa kujeruhiwa huku washambulianaji wakiwa hawana hofu na maisha ya wengine.
“Chanzo cha mzozo ni makabila ya Hausa yatanata kuundwa kwa mamlaka ya kiraia, sasa kundi hasimu linaona ni njia ya wenzao kupata ardhi sasa kila siku ni vita watu tunamalizika je Viongozi wetu wanafanya jitihada gani,” alihoji Kadir Jamaldin mkazi wa Garnis.
Naye, Haroub Ashraf anasema, “Tunasikia kwa wanahabari watu 31,000 wameyahama makazi yao, na wengi wanatafuta hifadhi katika shule ambazo zimegeuzwa kuwa kambi za wakimbizi sasa watoto watasoma wapi na tunaandaa taifa la namna gani? Viongozi wajitafakari hawatutendei haki tunateseka.”
Maandamano mengine yalitaka “umoja” na “kukomesha ukabila” katika taifa hilo maskini la kaskazini mashariki mwa Afrika, na licha ya mwishoni mwa Julai viongozi wakuu wa makundi hasimu kukubali kusitisha mapigano, lakini hali imekuwa ni tofauti.