Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimesisitizwa kuendelea kuimarisha umoja bila kujali mipaka ya nchi zao, ili kwa pamoja waweze kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazotokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Rai hiyo, imetolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya Mwenyekiti wake, Vita R. Kawawa katika ziara ya kutembelea miradi ya kikanda ya Barabara ya EAC, ambapo kwa pamoja wameitaja Jumuiya kuwa ni yenye maono na inayotafsiri mambo kwa vitendo.

Wajumbe hao, walielezwa uwepo wa miradi ya barabara zinazoiunganisha Tanzania na nchi tano za EAC ilizopakana nazo za Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo baadhi imekamilika, mingine kuwa katika hatua za ujenzi na mingine ikitafutiwa fedha za utekelezaji wake.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala, Mhandisi Steven Mlote (kushoto) akiongea wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), ilipotembelea Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mshariki, jijini Arusha. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya NUU, Vita R. Kawawa.

Aidha, wajumbe hao pia walielezwa namna Tanzania inavyoshirikiana na Sekretarieti ya EAC na nchi wanachama, kutekeleza miradi hiyo ya kimaendeleo kuanzia hatua ya uchambuzi yakinifu na baadaye kutafuta fedha za utekelezaji wake.

Waliitaja miradi michache, ambayo ipo katika ujenzi kuwa ni pamoja na barabara ya kutoka Kabingo, Kasulu hadi Manyovu (kilometa 260), inayounganisha Tanzania na Burundi na ile ya kutoka Tanga, Pangani, Saadan hadi Bagamoyo (kilomita 256), ikiunganisha Tanzania na Kenya.

Ujenzi wa barabara hiyo, utajumuisha pia daraja la Pangani la mita 500 huku upande wa Tanzania na Uganda ukiwa na mradi wa barabara ya Mutukula, Kiyaka, Kasulu hadi Benako (kilomita 124), na Bugene, Burigi, Chato hadi Kasulo (kilomita 68).

Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) wa Mkoa wa Arusha, Paul Kamukulu akifafanua utekelezaji wa majukumu ya Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Namanga, kwa wajumbe wa Kamati ya NUU walipotembelea kituo hicho Septemba 3, 2022.

Awali, wakikagua barabara ya kikanda ya Arusha, Namanga, Ath River na ile ya mzunguko ya Arusha, wajumbe hao walielezea namna ujenzi wake unavyounganisha nchi wanachama wa EAC, utakaochochea biashara, muingiliano wa watu na kuimarisha mtangamano wa EAC.

Katika ziara hiyo, pia wajumbe wa Kamati walitembelea Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Namanga na kisha kusikiliza mada kutoka kwa Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eliabi Chodota.

Miongoni mwa mada hizo, ni pamoja na ile iliyoelezea miradi mingine inayotekelezwa kwa uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, katika sekta za usafiri wa anga, reli, maji, hali ya hewa na nishati kwa nchi wanachama.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), wakifuatilia mada kuhusu utekelezaji wa miradi ya kikanda ya miundombinu ya EAC, iliyokuwa ikiwasilishwa na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eliabi Chodota (Hayupo pichani).

Ziara hiyo, iliratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ili kutoa fursa kwa wajumbe wa Kamati ya NUU kujionea baadhi ya miradi ya Jumuiya katika mikoa ya Dodoma, Manyara na Arusha iliyoanza Septemba 2 hadi 4, 2022.

Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eliabi Chodota akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa miradi ya kikanda ya miundombinu ya EAC, kwa wajumbe wa Kamati ya NUU jijini Arusha.

IGP aonya tabia ya kujichukulia sheria mkononi
Viongozi hawatutendei haki, tunateseka: Wananchi