Viongozi wa Dini Mkoani Mbeya, wametakiwa kutoa Elimu ya lishe kwa waumini wao, kwa lengo la kuhamasisha matumizi chakula na kuwa na afya bora, ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kitaifa na jamii kwa ujumla.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dkt. Maisara Karume ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa wadau wa masuala ya lishe na viongozi wa dini, ulioratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirikla lisilo la kiserikali la Helvetas Mkoani Mbeya.
Awali, katika Hotuba yake, Kaimu Mkurugenzi msaidizi wa kitengo cha Lishe Wizara ya Afya, Neema Joshua amesema lengo la kuwashirikisha viongozi wa dini ni kutengeneza ujumbe wa kuelimisha waumini hao kwa kuangalia mahusiano ya maneno yaliyoandikwa kwenye vitabu vya kiimani.
Nao baadhi ya Viongozi wa dini akiwemo Mch. Yared Nkoswe wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Nyanda za Juu Kusini, amesema kanisa limewekeza nguvu katika masuala ya afya, huku takwimu za Kitaifa za sasa zikionesha kuwa asilimia 30 ya watoto wenye umri chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa, asilimia 12 wana uzito pungufu na asilimia 3 wana ukondefu.