Baraza la Jeshi la Sudan inayoongoza nchi hiyo katika kipindi cha mpito imewakamata waliokuwa viongozi wa Serikali ya Omar Al-Bashir.
Jeshi hilo limeahidi kuwa litayafanyia kazi matakwa ya wananchi na halitawazuia raia kuandamana au kuwaondoa mitaani kwa nguvu, kwa mujibu wa CNN.
Hata hivyo, jeshi hilo limewashauri wananchi hao kuondoka mitaani ili nchi hiyo irejee katika hali ya kawaida na wao kuendelea na shughuli zao.
Msemaji wa jeshi hilo, Maj Gen Shams Ad-din Shanto ameutaka upande wa upinzani kumchagua Waziri Mkuu wao na kuahidi kuwa wataheshimu na kuufanyia kazi uamuzi wao.
“Baraza la kijeshi halitamchagua Waziri Mkuu, upande wa upinzani utamchagua na sisi tutazingatia na kuheshimu uamuzi wao,” alisema Shanto.
Miezi kadhaa baada ya maandamano nchini humo imesababisha kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa rais kwa miaka 30, Omar A-Bashir juma lililopita.
Waandamanaji wameahidi kuendelea kubaki mitaani hadi pale ambapo utasimikwa uawala wa kiraia nchini humo. Maelfu ya watu wamepiga kambi nchi ya jengo la wizara ya ulinzi jijini Khartoum.
Maandamano yalizuka kwa lengo la kupinga ugumu wa maisha wakitaka A-Bashir ajiuzulu. Jeshi la nchi hiyo liliamua kumuondoa madarakani kiongozi huyo wiki iliyopita, na kuahidi kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria nchini humo lakini sio kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).