Jeshi la polisi nchini Zimbabwe, jana liliwakamata viongozi wa vyama vya ushirika vya biashara wanaoratibu maandamano ya kupinga kodi mpya ya huduma za kutuma na kupokea fedha kieletroniki.
Vyama vya ushirika vya wafanyabiashara pamoja na vyama vya wafanyakazi vilitangaza kufanya maandamano kupinga hatua hiyo ya Serikali pamoja na kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma muhimu.
Polisi walikataa kuwapa kibali Zimbabwe Congress of Trade Unions (ZCTU) kufanya maandamano hayo, wakitoa sababu za kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, lakini umoja huo ulidai utaendelea na mpango wake.
Rais wa ZCTU, Peter Mutusa pamoja na Katibu Mkuu wake, Japhet Moyo wametajwa kuwa kati ya watu waliotiwa nguvuni na jeshi la polisi jijini Harare.
Aidha, Polisi waliweka ulinzi mkali katika maeneo ya mitaa ya Harare na kuwakamata baadhi ya wanaharakati waliokuwa wameanza kukusanyika katikati ya jiji.
Kwa mujibu wa Serikali ya Zimbabwe, kodi ya huduma za kifedha kwa njia ya kielectroniki itapanda kwa senti 2 kwa kila dola, kwa kila muamala utakaofanyika wenye thamani kati ya $10 hadi $500,000 kuanzia Oktoba 15 mwaka huu.