Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewasihi viongozi wa ngazi zote kufuatilia na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, ili kuhakikisha ahadi zilizotolewa zinatekelezwa katika maeneo yao.
Dkt. Mwinyi alitoa kauli hiyo katika mkutano wa viongozi wa CCM ngazi ya Shina, Majimbo, Wilaya na Mkoa wakati wa ziara yake ya kuimarisha chama na kutembelea miradi mbalimbali, uliofanyika katika ukumbi wa Picadilly, Kombeni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema, chama kinapaswa kuisimamia Serikali na kuzungumzia mambo mazuri yanayofanyika kwa wananchi. Utekelezaji wa miradi unaendelea, hivyo haiwezekani kwa chama tawala kushindwa kuongea kuhusu kufuatilia miradi ya maendeleo na utekelezaji wa ahadi zilizotolewa.