Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameitaarifu jamii hasa akina mama wajawazito wanaofika kwenye Kliniki za Uzazi, Mama na Mtoto kupimwa wingi wa damu, mkojo, wingi wa protini, shinikizo la damu pamoja na kusikiliza mapigo ya moyo ya mtoto bila kutozwa gharama zozote.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati wa kukabidhi vifaa tiba vya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa vituo ishirini vya Halmashauri za Mkoa wa Dodoma, vyenye thamani ya Shilingi milioni 45 .
Amesema, “ili kumuokoa mama mjamzito anapofika kliniki ni vyema kupimwa vipimo hivyo muhimu, vipimo hivi vyote ni bure na ni lazima viwepo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vyote nchini.”
Aidha, Ummy ameongeza kuwa Serikali itahakikisha upatikanaji wa dawa za kuzuia kutoka damu wakati wa kujifungua, dawa za kuongeza damu na dawa za kuzuia kifafa cha mimba katika vituo vya afya vya umma nchini kwa asilimia 100.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatimiza wajibu wake kwa kujenga majengo,kuboresha miundombinu, kuongeza ajira pamoja na kununua vifaa tiba , hivi sasa tunapata fedha za dawa kila mwezi shilingi bilioni 20, tutahakikisha hizi dawa tatu zitapatika kwa asilimia 100,” amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo, amezitaka Timu za afya za uendeshaji za Halmashauri nchini kufanya usimamizi shirikishi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuwajengea uwezo watoa huduma za afya.
Amesema, “huu ndio muelekeo wa wizara, twende kwenye masuala ya kuwawezesha wataalamu wetu kwenye vituo vya afya na kuona kipi kinafanyika tunaweza kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga kama tutaongeza kutoa huduma bora za afya.”
Aidha amezitaja taarifa za Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya na Utafiti wa Kiashiria cha Malaria (DHS/MIS) ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa nchi imepiga hatua katika viashiria vingi vya afya vya mama na mtoto mathalani vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimeshuka kutoka 67 kati ya vizazi hai 1000 mwaka 2015/2016 hadi 43 kwa kila vizazi hai 100.