Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya utafutaji wa mafuta, ili kuchangia maendeleo ya nchi, ambapo tangu kupatikana kwa uhuru mpaka sasa jumla ya visima 96 vya utafutaji wa mafuta vimechimbwa nchi kavu na baharini, na visima 44 kati ya hivyo imegundulika gesi asilia.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni ameeleza hayo katika hotuba yake ya mafanikio na maendeleo ya PURA katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania, leo Novemba 19, 2021, Jijini Dar es Salaam.
“Mwaka 1952 kulikuwa na kisima kimoja tu kilichochimbwa katika utafutaji wa mafuta, lakini mpaka sasa jumla ya visima 96 vimechimbwa, nchi kavu visima 59 na baharini visima 37, ambapo visima 44 kati ya hivyo, imegundulika gesi asilia,” alisema Mhandisi Sangweni.
Aliendelea kusema kuwa, katika visima 44 vya gesi asilia vilivyogunduliwa, visima 16 ni vya nchi kavu na visima 28 ni vya baharini. Ametaja maeneo yenye visima hivyo, kuwa ni Ruvu na Mkurunga mkoani Pwani, Ntorya na Mnazibay (Kijiji cha Msimbati) mkoani Mtwara pamoja na Songo Songo mkoani Lindi.
“Ugunduzi wa gesi asilia umewezesha kuanza kutumika kwa gesi asilia kama chanzo cha nishati, hususan kwa kuzalisha umeme viwandani, majumbani na kwenye magari,” amesema Mhandisi Sangweni.
Aidha, ameeleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuimarika kwa mifumo ya udhibiti, kisheria na kitaasisi nchini, ambapo kumekuwepo na sheria ya Petroli ya mwaka 1980, Sera ya Nishati ya mwaka 2015, Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 na Sheria ya Udhibiti wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015 pamoja na uanzishwaji wa PURA, EWURA na TPDC.
“Sheria hizi zimepelekea nchi kuwa na mikataba ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji mafuta na gesi asilia (PSA) ipatayo 11, kati ya hiyo Mitatu (3) ipo katika hatua ya uzalishaji wakati mikataba Nane (8) ipo katika hatua mbalimbali za utafutaji,” amesema Mhandisi Sangweni.
Ameendelea kusema kuwa, kupatikana kwa mikataba 11 ni mafanikio makubwa katika utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi, kwani kabla ya uhuru hakukuwa na mkataba wowote uliosainiwa ila nchi ilikuwa inafanya maridihiano na wawekezaji.
Mafanikio mengine, yaliyopatikana katika sekta hiyo ni pamoja na uajiri wa Watanzania katika nafasi mbalimbali kwenye kampuni za gesi asilia umeongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi pamoja na kuimarika kwa shughuli za kaguzi za gharama za matumizi katika mikataba ya gesi asilia, ambapo kaguzi hizo zimeokoa zaidi ya shilingi bilioni 90.