Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Wafanyabiashara na wawekezaji Nchini Singapore, amewakaribisha wawekezaji hao kuwekeza nchini hasa katika sekta za viwanda, kuwekeza na kuweka ushirikiano katika sekta ya bandari hasa katika miundombinu ya bandari,usafiri pamoja na mifumo ya Tehama.

Dkt. Mpango amesema serikali imeendelea kuweka mkazo katika uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa  kutunga sera na kufanya marekebisho ya sheria zinazorahisisha ufanyaji biashara pamoja na kutatua changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara kupitia Baraza la Biashara la Taifa ambalo huongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha Dkt. Philip Mpango ametaja hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuweka mazingira salama ya uwekezaji ikiwemo kuendeleza miradi mikubwa itakayotoa unafuu katika kuwekeza kama vile Ujenzi wa mradi wa Umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (JNHPP), Ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR),Kuboresha shirika la ndege ambapo mpaka sasa jumla ya ndege 11 zimekwisha nunuliwa,kuboresha bandari, kuwekeza katika kutoa nishati vijijini, kuboresha miundombinu pamoja na huduma za kijamii. 

Dkt. Mpango amewakaribisha wawekezaji hao katika sekta ya utalii kuwekeza katika miundombinu yake ikiwemo hoteli na  kumbi za mikutano.

Makamu wa Rais amewahakikishia wawekezaji hao kwamba Tanzania itaendelea kuimarisha amani na utulivu ili kulinda biashara pamoja na uwekezaji uliofanyika kutoka ndani na nje ya nchi.

Wafanyabiashara hao wamemueleza Makamu wa Rais nia yao ya kuwekeza nchini Tanzania na kuiomba serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kuondoa vikwazo hasa katika masuala ya biashara ya kilimo, kuongeza ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na kuomba kuendelea kuimarika kwa ushirikiano baina ya Tanzania na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kurahisisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa zitakazozalishwa.

Visima 44 vya gesi asilia vimegunduliwa
IGP Sirro awaonya wavuruga amani