Uongozi wa Klabu ya Arsenal umeanza maandalizi ya kuziba nafasi ya Meneja wa klabu hiyo Mikel Arteta, anayetajwa kuwindwa na Mabingwa wa Soka nchini Hispania Real Madrid.
Uongozi wa The Gunners umeripotiwa kuwa katika mpango wa kumshawishi Meneja wa Brighton, Roberto De Zerbi kama mbadala wa Arteta ambaye amekuwa na msimu mzuri katika Ligi ya England, akikaribiwa kuipa taji klabu hiyo ya Kaskazini mwa London.
Arsenal inayoongoza Ligi Kuu England, inaripotiwa kuihofia Madrid itamfuata Arteta huku FC Barcelona ipo mbioni kubeba ubingwa wa La Liga msimu huu, lakini inasemekana Inter Milan nayo inavutiwa na De Zerbi, raia wa Italia.
De Zerbi, Meneja wa zamani wa Sassuolo na Shakhtar Donetsk, mwenye umri wa miaka 43, ameiongoza vyema Brighton akiipandisha hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu 2022/23.
Taarifa mbalimbali za magazeti kutoka England zimeripoti kuwa Arsenal itajiandaa kufanya chaguo bora la kocha endapo itampoteza Arteta siku za usoni.
Arteta ameiongoza Arsenal kukaa kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya alama nane dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City, huku ikiwa katika mbio za kuwania ubingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004.
Imeelezwa De Zerbi atakuwa chaguo sahihi endapo Arteta ataondoka kutokana na uzoefu wake kwenye Ligi Kuu England. Hata mashabiki wanavutiwa na De Zerbi.
Real Madrid inatajwa kuwa katika mpango wa kumsaka Meneja wa kikosi chao, ikipanga kuachana Carlo Ancelotti anayetajwa kuwindwa na Shirikisho la Soka nchini Brazil CBF, ili kukinoa kikosicha timu ya taifa hilo.