Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mkakati wa Serikali ni kumwezesha kila Mtanzania apate kitambulisho cha Taifa akiwa kijijini kwake na kwamba kitambulisho hicho ni cha Taifa, na kinahusu usalama wa Tanzania, hivyo asingependa asiye raia awe nacho kwani ni mali ya Watanzania.

Majaliwa ameyasema hayo leo Mei 11, 2023 bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhandisi Ezra Chiwelesa kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Amesema, Serikali inaendelea na zoezi la utoaji wa vitambulisho kupitia taasisi ya NIDA ambayo awali ilikuwa na changamoto ya upungufu wa watumishi lakini hivi sasa imeshatatuliwa na kwamba awali kulikuwa na idadi ndogo ya watumishi wa kuweza kuwafikia wananchi.

“Kwa sasa tumeongeza idadi ya watumishi na ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuipongeza Serikali kwani vitambulisho vinatolewa kwa wingi na inawezekana kabisa wale ambao hawajafikiwa na hasa kwenye mikoa ya pembezoni, ni kutokana na kuwepo kwa changamoto ya muingiliano wa mataifa ya jirani.” amesema Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alitaka kujua ni kwa nini Serikali haioni haja ya kuanza mchakato wa kuhuisha vitambulisho vya Taifa kama ilivyofanya kwenye zoezi la awali kwa kuwa kuna vijana wengi ambao wamefikisha umri wa miaka 18 na hawakupata fursa ya kujiandikisha kwenye awamu ya kwanza kwa hiyo hawana vitambulisho hivyo kama sera inavyotaka ikiwemo wananchi wa mikoa ya pembezoni.

TAQA yaahidi kujenga vituo 12 vya usambazaji gesi asilia
Baba Messi amkingia kifua mwanawe PSG