Serikali Nchini, imepata Shilingi 3.3 bilioni kwa kuuza lita 272, 444 za viuatilifu vya vya kuua mazalia ya Mbu kwa nchi saba za Afrika za Kenya, Angola, Niger, Botswana, Namibia Msumbiji na Swatini huku mazungumzo na nchi ya Uganda ikiwa kwenye mazungumzo ya kununua dawa hiyo, kupitia kiwanda cha Tanzania Biotech Products Ltd – TPBL.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Ashatu Kijaji wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuelezea mafanikio mipango na mikakati ya kiwanda hicho kinachojihusisha kuzalisha viwatilifu vya kuuwa mazalia ya mbu ambacho kiko chini ya Shirika la Maendeleo ya Taifa – NDC, kilichopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.
Amesema, “tunataka hii ndiyo iwe bidhaa itakayoitangaza Tanzania kwa kuuzwa nchi jirani na Afrika nzima kupitia eneo huru la biashara ambapo kuna nchi 54 ambapo bidhaa zitaingia kwenye soko hilo bila ya kodi na tozo ambapo majadiliano bado yanaendelea.”
Dkt. Kijaji ameongeza kuwa tayari mamlaka udhibiti mimea imetoa cheti cha usajilihuku akitoa siku tano kwa Shirika la Viwango Nchini – TBS, kukamilisha ithibati ya dawa hiyo kuwa kwenye viwango vinavyotakiwa pia itambuliwe na viwango vya kimataifa ISO ili nchi iweze kuhudumia dunia kwa kilimo kwani matumizi ya viuatilifu hivyo ni salama kwa chakula.
“Kitengo cha masoko kijiangalie kwani kiwanda kinapaswa kijiendeshe kwani ni cha kibiashara siyo cha huduma kwani kinatakiwa kizalishe bidhaa bora serikali ipate mapato nataka taarifa ndani ya siku 14 nipate majibu na hatutatoa tena maelekezo bali tutakuwa tofauti,” amesema Dkt. Kijaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa NDC Dk Nicoluas Shombe amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalishaji dawa hiyo milioni sita kwa mwaka huku Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, DkT. Lugano Wilson akisema watayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa.