Vyama vya upinzani nchini Israel, vimekubaliana kuunda serikali mpya, na hii inamaanisha kuwa uongozi wa muda mrefu wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa miaka 12 unafika mwisho.
Kiongozi wa chama cha Yesh Atid cha mrengo wa kati Yair Lapid, ametangaza hatua hiyço baada ya vyama nane vya upinzani kukubali kuja pamoja na kuunda serikali hiyo mpya.
Wanasiasa hao wa upinzani wamekubaliana kuwa nafasi ya Waziri Mkuu miongoni mwao itakuwa kwa mzunguko, na kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia cha Yamina, Naftali Bennet, ndiye ataanza kushika madaraka hayo kabla ya kumkabidhi Bwana Yair Lapid.
Baada ya makubaliano hayo, Bwana Lapid amesema kuwa amemwarifu rais Reuven Rivlin kuwa amefanikiwa kuunda serikali ambayo ameeleza kuwa itawatumikia Waisraeli wote.
Kabla ya kuanza kazi, serikali hii mpya, itapigiwa kura na wabunge ili kuidhinishwa.
Iwapo serikali hiyo itashindwa kupata uungwaji mkono wa Wabunge 120, basi itawazalimu Waisraeli wapige tena kura, utakuwa ni uchaguzi wa tano ndani ya miaka miwili ili kupata serikali.
Netanyahu amesema, makubaliano ya kuundwa kwa serikali hii mpya, kunahatarisha usalama wa Israel, baada ya chama chake cha Likud kushindwa kuunda serikali.