Spika wa Bunge Job Ndugai amesema uvumilivu wa chombo hicho kwa waandishi wa habari wanaopotosha taarifa za Bunge umefikia mwisho hivyo ataanza kushughulika nao kwa kuwafikisha kwenye Kamati ya Maadili.
Ametoa kauli hiyo leo Juni 25, 2021 Bungeni Jijini Dodoma amesema Bunge limekuwa na uvumilivu kwa muda kwa baadhi ya vyombo vya habari alivyosema vina mlengo wa tofauti na shughuli za taasisi hiyo.
“Kamati yetu iko imara, utafika wakati lazima wahusika waanze kuitwa mbele ya Kamati yetu na hatua zichukuliwe kukomesha tabia hiyo,” amesema Spika.
Mbunge wa Kibamba Issa Mtemvu ambaye aliomba kujua kuhusu upotoshaji uliofanywa na moja ya chombo cha habari dhidi yake.
Katika mwongozo wake Mtemvu ameeleza kuwa jana wakati akichangia bungeni alitaka kujua kuhusu mgawanyo wa mali za lililokuwa Jiji la Dar es Salaam lakini kuna chombo kilimnukuu vibaya na kimesababishia usumbufu.
Spika Ndugai amesema watafuatilia jambo hilo na kilichoandikwa katika chombo hicho cha habari ili kujua ukweli wake na ndipo atalitolea maamuzi ya nini kifanyike.