Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu wanapowasilisha taarifa za kiutumishi ili kuepuka malalamiko yanayohusu stahili mbalimbali za kiutumishi.

Ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Umma mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kuzungumza na Watumishi wa Umma mkoani humo kuhimiza uwajibikaji.

Amesema kuwa zoezi la kusafisha taarifa za watumishi limeibua kero kwa baadhi ya watumishi kutokana na waajiri kutozingatia maadili wanapowasilisha taarifa za kiutumishi.

“Awali baadhi ya waajiri waliwasilisha taarifa za watumishi zisizo sahihi hali iliyosababisha baadhi ya watumishi hao kupewa stahili ambazo si halali na matokeo yake wakati wa zoezi la kusafisha taarifa wamekuwa wakibainika kutostahili na hatimaye watumishi hao kuona kama wameonewa,” amesema Dkt. Mwanjelwa

Aidha, ameongeza kuwa, mtumishi wa umma anakamilika kwa kuwa na tabia njema, nidhamu ya kazi, mwenendo mzuri, weledi na ubunifu, hivyo ni vyema kila mtumishi akazingatia hilo ili awe na manufaa kwa umma na tija kiutendaji.

Hata hivyo, amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha utumishi wa umma unakaa sawa, kama mtumishi anapaswa kupata haki yake, atapata na kama hastahili aachwe badala ya kupendelewa.

 

Video: Viongozi Chadema walivyotumia msiba kufikisha kilio chao, Polisi yatoa msimamo usafiri mabasi saa 24
Dkt. Bashiru awaonya viongozi wa CCM na Serikali, 'Atakayewadharau hawa huyo hatufai'